Cheti cha kuzaliwa ni hati muhimu sana. Kama mzazi au mlezi, unapaswa kuhakikisha kuwa mtoto wako amepewa hati hii ya kujitambulisha.

Kila mtu anahitaji cheti cha kuzaliwa wakati anafanya maombi anuwai kama vile kuomba Kitambulisho cha Kitaifa, kujisajili kwa mitihani ya Cheti cha Kenya cha Elimu ya Sekondari na cha Elimu ya Msingi (KCSE na KCPE). Hati hiyo pia inahitajika wakati mtu anaomba pasipoti na maombi mengi zaidi ya serikali.

Kwenye nakala hii, tutakuelezea jinsi unavyoweza kupata cheti cha kuzaliwa kwa mtoto aliyezaliwa hospitalini na pia jinsi ya kupata cheti hicho kwa kesi za wale waliozaliwa nyumbani.

 

Jinsi ya kupata cheti cha kuzaliwa kwa mtoto aliyezaliwa hospitalini.

Hii inatumika pale ambapo mama alijifungua mtoto katika kituo cha afya kinachotambuliwa. Mchakato wa kupata cheti cha kuzaliwa huanza hospitalini ambapo mtoto alizaliwa

Kwa watoto waliozaliwa katika hospitali zilizo katika kambi za wakimbizi nchini Kenya (Kakuma na Dadaab), mchakato wa kupata cheti cha kuzaliwa ni kama ifuatavyo;

  • Muuguzi au mfanyikazi aliyeteuliwa hospitalini atajaza maelezo ya mtoto aliyezaliwa katika Fomu ya B1 ('Sajili ya Kuzaliwa') kwa nakala (ili kuwe na nakala mbili.)
  • Mama / baba au ndugu wa karibu (mwombaji) atapewa sehemu ya JUU ya Fomu ya B1 ambayo ina rangi ya waridi. Hii inajulikana kama Kukubaliwa kwa Arifa ya Kuzaliwa (ABN).

- Hakikisha unapata ABN kabla ya kuondoka kwenye kituo cha afya ambapo mtoto alizaliwa.

- ABN hutolewa bure.

  • Hospitali itahifadhi maelezo ya nakala ya ABN kama sehemu ya kumbukumbu za usajili wa kituo cha afya. Wafanyakazi wa hospitali pia huweka kwa muda sehemu ya CHINI (asili na nakala) ili waiwasilishe baadaye kwa Idara ya Usajili wa Umma (DCR) na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) kwa sababu za takwimu.
  • Wafanyakazi wa Hospitali watawasilisha maelezo ya usajili wa kuzaliwa kwa kujaza fomu itakayopelekwa UNHCR na DCR kwa sababu za takwimu.
  • Idara ya Usajili wa Umma utapata sajili za kuzaliwa kutoka UNHCR na kutengeneza vyeti vya kuzaliwa kisha kuzitoa kwa UNHCR
  • UNHCR inawasilisha vyeti vya kuzaliwa kwa waombaji.

B1_Form_-_Swahili.png

Ikiwa mtoto alizaliwa hospitalini nje ya kambi za wakimbizi (kama vile Nairobi, Mombasa na kadhalika), mzazi au mlezi anayeomba cheti cha mtoto huyo cha kuzaliwa lazima awasilishe nakala ya sehemu ya ABN / Sehemu ya juu ya Fomu ya B1 (yenye rangi ya waridi) kwa Idara ya Usajili wa Umma (DCR). Hati hii pia ilitolewa kwa DCR kutoka kituo cha afya alikozaliwa mtoto.

 

Mara tu watakapopokea hati hiyo, DCR watafanya upekuzi katika hospitali hiyo na kisha kutoa Cheti cha Kuzaliwa kwa mwombaji baada ya kuthibitisha kuwa mtoto huyo alizaliwa katika hospitai hiyo.

 

Jinsi ya kupata cheti cha kuzaliwa kwa mtoto aliyezaliwa nyumbani

Mchakato wa kupata cheti cha kuzaliwa kwa mtoto aliyezaliwa nyumbani ni tofauti kidogo na ile ya watoto waliozaliwa katika kituo cha afya.

Ni muhimu kukumbuka kuwa chini ya sheria za Kenya, mtoto aliyezaliwa nchini Kenya anapaswa kusajiliwa kwa cheti cha kuzaliwa mara tu baada ya kuzaliwa au ndani ya miezi sita (6) baada ya kuzaliwa. Hii inasamehewa tu wakati msajili amepata idhini kutoka kwa Msajili Mkuu na baada ya malipo ya ada ya usajili iliyochelewa.

Ikiwa mama atajifungua nje ya kituo cha afya (kwa mfano nyumbani, kando ya barabara na kadhalika), itafikiriwa kuwa mama amekuwa akihudhuria kliniki za utunzaji wa wajawazito (ANC) ndani ya kambi au nje ya kambi kabla ya kujifungua.

Hii inamaanisha kuwa wanatarajiwa kuwa na kijitabu cha kliniki / kadi / rekodi inayothibitisha kwamba wamekuwa wakipokea huduma za utunzaji wa ujauzito (ANC) na wanapaswa kuwa na kijitabu au kadi halali ya kliniki ya ANC.

Hapa kuna hatua za kufuatwa kupata cheti cha kuzaliwa kwa mtoto aliyezaliwa nyumbani.

  • Mama wa mtoto au mwombaji anapaswa kuwa na kijitabu / kadi ya kliniki inayojulikana kama 'Kijitabu cha Afya ya Mama na Mtoto' (Kitabu cha Zambarau) na hati zake za utambulisho. Hii inaweza kuwa Kitambulisho cha Wakimbizi, pasipoti au Dhibitisho la Usajili. Anapaswa kuipeleka kwa Idara ya Usajili wa Kiraia katika kiwango cha kambi.
  • Idara ya usajili wa umma utamtaka mwombaji (pamoja na mtoto) kuwapo na watapokea hati zinazohitajika. Baada ya kupokelewa, nyaraka zitachunguzwa, na maelezo ya mtoto kuhusu uzazi, jina, jinsia, umri / tarehe ya kuzaliwa, na mahali pa kuzaliwa yatathibitishwa.
  • Mara tu idara ya usajili wa umma ikithibitisha ushahidi kuunga mkono maombi ya usajili wa kuzaliwa, watajaza na kusaini Fomu ya B1 kwa nakala; mwombaji atapewa sehemu ya Juu ya Fomu ya B1 yaani Kukubaliwa kwa Arifa ya Kuzaliwa (ABN), na Idara ya Usajili wa Umma (DCR) itasalia na nakala kama sehemu ya kumbukumbu za usajili wa kuzaliwa huku nakala ingine ikisalia na UNHCR kwa kumbukumbu zake.
  • Usajili wa uma utatayarisha Cheti cha Kuzaliwa. Vikiwa tayari, vyeti hivyo vitatumwa kwa UNHCR.
  • UNHCR inawasilisha vyeti vya kuzaliwa kwa waombaji.

Idara ya usajili wa umma inapatikana wapi kambini?

Afisa wa Huduma ya Usajili wa umma hutembelea kambi mara kwa mara kusuluhisha maswala ya usajili. UNHCR na RAS mara nyingi hutoa maelezo kuhusu ni lini maafisa hao wanapatikana na Julisha.Info itatoa habari hizo kupitia ukurasa wetu wa Facebook.

 

Iwapo una maswali yoyote, wasiliana nasi kupitia ukurasa wa Julisha.Info kwenye mtandao wa Facebook, kila Jumatatu hadi Jumamosi kutoka saa 2 asubuhi hadi saa 11 jioni.