Wakimbizi, waosihi hifadhi, na wageni wanaoishi Kenya wana haki ya kupata huduma muhimu zinazotolewa na serikali kuu na serikali za kaunti. Serikali ya Kenya ina tovuti moja ya mtandao kwa huduma zote za serikali, inayojulikana kama eCitizen. Jukwaa hili la mtandao limeundwa ili kurahisisha na kuharakisha mchakato wa kuomba huduma mbalimbali. Tovuti ya eCitizen ndiyo jukwaa kuu la kufikia zaidi ya huduma za serikali 16,000. Tovuti hii ilizinduliwa mwaka 2014 ili kusaidia raia, wageni wanaotembelea Kenya, wakaazi wasio Wakenya, na wakimbizi. Baadhi ya huduma za kawaida zinazopatikana kwenye eCitizen ni pamoja na:
- Maombi ya usajili wa vikundi vya kijamii
- Usajili wa biashara kwa Wakenya, wakimbizi, na wageni
- Maombi ya vyeti vya kuzaliwa
- Maombi ya leseni ya kuendesha gari
- Maombi ya cheti cha maadili au kibali cha polisi
- Maombi ya vyeti vya ndoa
- Uwasilishi wa marejesho ya kodi na huduma nyingine za Mamlaka ya Mapato nchini (KRA), miongoni mwa zingine.
Mtu anatakiwa kuunda akaunti kwenye eCitizen kwa kutumia nyaraka zao za utambulisho. Raia wa Kenya wanatakiwa kutumia Kitambulisho cha Taifa, wakaazi wanatumia Kitambulisho cha Mgeni (Alien ID), wageni wanaotembelea Kenya wanatumia pasi zao za kusafiria, na wakimbizi wanatumia Kitambulisho cha Wakimbizi. Jukwaa hili pia lina mfumo wa malipo, unaoruhusu kulipia huduma kupitia pesa za simu (M-Pesa), kadi za mkopo, na uhamisho wa benki.
Manufaa ya Akaunti ya eCitizen
Jukwaa la eCitizen limewafanya watu kuwa na urahisi wa kufikia huduma mbalimbali mara moja:
- Urahisi: Kwa kuwa jukwaa hili liko mtandaoni, watumiaji wanaweza kupata huduma wakati wowote, popote walipo, bila kujali tofauti za saa , na hivyo kuepuka foleni na urasimu usio wa lazima.
Ufuatiliaji: Inawawezesha watumiaji kufuatilia hali ya maombi yao, na hivyo kukuza uwazi katika utoaji wa huduma. - Gharama Nafuu: Inapunguza gharama za safari na za kiutawala, kwa kuwa watumiaji wanaweza kukamilisha shuguli yote mtandaoni.
- Kuongeza kasi ya usindikaji: Huwezesha huduma kama vile kuomba vibali, pasi za kusafiria, usajili upya wa vitambulisho, vyeti vya kuzaliwa, na usajili wa biashara kufanyika kwa haraka zaidi.
Vigezo vya Kustahiki kwa Akaunti ya eCitizen
Ili kufuzu kuwa na akaunti ya eCitizen nchini Kenya, wakimbizi, waosihi hifadhi, wageni, na raia wanapaswa kufikia vigezo vifuatavyo:
- Mtu lazima awe na umri wa miaka 18 au zaidi.
- Raia wa Kenya wanatakiwa kuwa na Kitambulisho cha Taifa (ID) kilicho halali.
- Wakimbizi wanatakiwa kuwa na Kitambulisho cha Wakimbizi kinachotambuliwa au Kitambulisho cha Mgeni.
- Wakaazi wa kigeni wanahitaji Kitambulisho cha Taifa cha Kigeni kilicho halali kinachotolewa na Idara ya Uhamiaji ya Kenya.
- Wanadiplomasia wanahitaji Kitambulisho cha Kidiplomasia kinachotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje (MFA) nchini Kenya.
- Nambari halali ya simu ya mkononi na anwani ya barua pepe zinahitajika kwa uthibitisho wa akaunti na taarifa kutoka kwa jukwaa la eCitizen.
- Mtu lazima awe na ujuzi wa kutumia kompyuta na aweze kusoma na kuandika kwa Kiingereza ili kutumia jukwaa hili kivyake. Katika miji mingi na vituo vya kibiashara nchini Kenya, baadhi ya biashara binafsi hutoa kompyuta kwa ajili ya kupata huduma za mtandao na msaada kwa huduma hizi kwa malipo.
Jukwaa hili linatoa orodha kamili ya huduma zote zinazotolewa na serikali. Huduma zimeorodheshwa chini ya idara au wizara maalum za serikali ya kitaifa na kaunti.
Mwongozo wa Hatua kwa Hatua Jinsi ya Kuunda Akaunti ya eCitizen kama Mkimbizi Nchini Kenya
Ili kuunda akaunti ya eCitizen kama mkimbizi nchini Kenya, fuata hatua zilizo hapa chini. Ni lazima uwe na:
- Kadi ya Utambulisho ya Mkimbizi iliyotolewa na Serikali ya Kenya (Idara ya Masuala ya Wakimbizi au UNHCR) kwa ajili ya utambulisho.
Hatua ya 1: Tembelea Tovuti ya eCitizen, kisha uende kwenye jukwaa la eCitizen .
Hatua ya 2: Sajili akaunti yako kwa kuchagua ‘Refugee’ chini ya aina za akaunti.
Weka Nambari yako ya Kitambulisho cha Mkimbizi na maelezo mengine yanayohitajika (anwani ya barua pepe, nambari ya simu, n.k.), kisha fuata maagizo yanayoonekana kwenye simu/tarakilishi yako.
Hatua ya 3: Uthibitisho wa Maelezo ya Akaunti Yako
Utapokea ujumbe mfupi kutoka ‘ECITIZEN’ wenye tarakimu sita ambao utaandika kwenye jukwaa ili kuthibitisha akaunti yako. Tarakimu huu pia utatumwa kwenye anwani ya barua pepe uliyoitumia kusajili kwenye jukwaa.
Hatua ya 4: Anzisha Akaunti Yako
Hii ni hatua ya mwisho. Baada ya kuthibitisha akaunti yako, mfumo utaweza kuanzisha wasifu wako kwenye jukwaa. Sasa unaweza kutafuta na kufikia huduma kama vile vibali, leseni, na huduma nyingine zinazotolewa kwa wakimbizi.
KWA WAKENYA:
- Tembelea Tovuti ya eCitizen: Nenda kwenye jukwaa la eCitizen: Katika jukwaa, upande wa kulia, bonyeza kitufe cha kijani kilichoandikwa ‘Register’ ili kuendelea.
- Bonyeza ‘Create Account’ na Chagua ‘Kenyan Citizen’: Baada ya kubonyeza ‘Register’, chagua aina ya akaunti ili kuendelea na hatua. Kwa raia wa Kenya, chagua aina ya akaunti ya ‘Citizen’ na jaza maelezo kama jina la kwanza, nambari ya Kitambulisho, na mwaka wa kuzaliwa, kisha fuata maagizo yanayoonekana. Hakikisha maelezo ni sahihi kabla ya kubonyeza kitufe cha ‘Validate’
- Weka Anwani Yako ya Barua Pepe na Nambari ya Simu: Baada ya kuthibitisha maelezo, jina lako kamili litaonekana pamoja na Kitambulisho. Endelea kujaza maelezo sahihi ya mawasiliano, kama vile nambari ya simu halali (anza na +254...) na anwani ya barua pepe, kisha fuata maagizo yanayoonekana.
- Uthibitisho: eCitizen inahitaji kila mtu kuthibitisha utambulisho wao kwa kutumia msimbo wa siri wa mara moja (verification code) ambao unatumwa kupitia barua pepe au SMS. Ingiza msimbo wa uthibitisho ili kukamilisha usajili.
- Unda neno la siri na Kubali Masharti: Baada ya kuingiza msimbo wa siri wa mara moja uliopewa, bonyeza hatua inayofuata kuunda neno lako la siri la chaguo lako kulingana na maagizo.
- Weka Picha ya Pasipoti Yako & Kubali Masharti ya Huduma: Katika hatua hii, unatakiwa kuweka picha ya pasipoti yako ambayo itasaidia katika kuimarisha taarifa zako binafsi. Kukubali masharti ya huduma kunathibitisha pia kuwa unakubaliana na masharti na vigezo vilivyowekwa na Serikali ya Kenya kuhusu maombi haya.
- Anzisha Akaunti Yako: Baada ya kuthibitishwa, ingia kwenye akaunti yako ili kufikia huduma mbalimbali za serikali unazohitaji.
Kuunda Akaunti ya eCitizen kama Mwanadiplomasia Nchini Kenya
Kupata jukwaa la eCitizen nchini Kenya kama mwanadiplomasia kunahitaji hatua tofauti kidogo na mchakato wa kawaida wa raia au wakaazi wa kigeni.
Wanadiplomasia nchini Kenya wanaweza kuunda akaunti kwenye jukwaa la eCitizen kwa kuchagua chaguo maalum kwa wanadiplomasia kwenye ukurasa wa usajili.
Mahitaji ya Akaunti ya eCitizen kwa Mwanadiplomasia
Ili kujisajili, wanadiplomasia wanahitaji kuwa na:
- Kitambulisho cha Kidiplomasia kinachotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje (MFA) nchini Kenya.
- Anwani ya barua pepe halali na nambari ya simu kwa ajili ya uthibitisho na mawasiliano.
- Upatikanaji wa mtandao.
Huduma Zinazopatikana kwa Wanadiplomasia kwenye eCitizen
- Huduma za Uhamiaji
- Usajili wa magari
- Maombi ya viza na huduma nyingine za serikali.
Kumbuka: Baadhi ya huduma bado zinaweza kuhitaji kutembelea ofisi maalum za serikali ana kwa ana, kulingana na aina ya ombi.
Kuunda Akaunti ya eCitizen kama Mkaazi wa Kigeni Nchini Kenya
Ili kuunda akaunti kama mkaazi wa kigeni, tembelea tovuti ya eCitizen na fuata hatua zilizo hapa chini:
- Katika ukurasa wa kwanza, bonyeza "Create Account."
- Chagua Foreign Residents. Hii ni kwa ajili ya raia wa kigeni wanaoishi Kenya ambao wana
- Kitambulisho cha Taifa cha Kigeni kilichotolewa na Idara ya Huduma za Uhamiaji.
- Andika maelezo yanayohitajika na fuata maagizo yanayoonekana.
- Toa maelezo mengine yanayohitajika, kama vile anwani yako ya barua pepe na nenosiri salama, ambalo litatumika kufikia akaunti yako.
Soma zaidi kuhusu huduma za serikali zilizoainishwa kwenye ramani zetu za huduma za Julisha.Info kwa kubonyeza viungo vilivyo hapa chini:
Department of Immigration Services
Department of Refugee Services
Child welfare society of Kenya, Lodwar
Ikiwa una maswali yoyote, tafadhali tuandikie kupitia ukurasa wa Facebook wa Julisha.Info au zungumza nasi kupitia WhatsApp (+254110601820) ,Jumatatu hadi Ijumaa kutoka 08:00 asubuhi hadi 5:00 jioni