Watoto wanaoishi vijijini na mijini wanaweza kukumbana na changamoto mbalimbali kutokana na mambo kama hali ya kijamii na kiuchumi, unyanyapaa na ubaguzi, mienendo ya familia, na ukiukwaji wa haki zao na watu wa karibu. Ukatili dhidi ya watoto, hasa ajira ya watoto, umeenea zaidi katika familia zinazokabiliwa na umaskini na uhaba wa rasilimali. Kaya na familia zilizo maeneo kama kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma pamoja na jamii zinazozunguka maeneo hayo ya ukame na nusu-ukame ziko katika hatari zaidi kutokana na kipato cha chini, kuhama kwa sababu ya ghasia/mizozo na hali mbaya ya hewa kama ukame unaoathiri upatikanaji wa chakula. Kutokana na hayo, watoto wengi wanalazimika kufanya kazi ili kusaidia wazazi wao na walezi kutimiza mahitaji yao ya msingi kama chakula. Hii inasababisha baadhi ya watoto kuacha shule ili waweze kupata kipato kwa njia ya kazi.
Katika makala hii, tumetoa taarifa zilizothibitishwa ili kukusaidia kuelewa ajira kwa watoto, jinsi inavyowaathiri watoto, na mashirika yanayotoa huduma za kukabiliana na ukatili, kutelekezwa, unyanyasaji, na ukatili dhidi ya watoto. Kuelewa sababu za ajira ya watoto na kufanya juhudi ili kumaliza desturi hii ni muhimu kwa ustawi wa watoto wetu. Kila mtu katika jamii ana jukumu la kutengeneza mazingira salama yasiyokuwa na ajira kwa watoto na ukiukwaji wa haki za watoto.
Mtoto ni nani?
Kulingana na Shirika la Umoja wa kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Sheria nchini Kenya, mtoto ni mtu yeyote aliye na umri wa chini ya miaka 18.
Ajira kwa Watoto ni nini ?
Ajira kwa watoto ni aina yoyote ya kushiriki katika kazi kwa njia ambayo inawanyima watoto nafasi ya kufurahia utoto wao, kufikia uwezo wao, na kuhifadhi hadhi yao, na ambayo ni hatari kwa maendeleo yao ya kimwili na kiakili. Kulingana na shirika la kazi duniani (ILO) na UNICEF, ajira ya watoto inahusisha kazi ambayo watoto ni wadogo sana kuifanya au ambayo, kwa asili yake au hali zake, inaweza kuzingatiwa kuwa isiyo salama. Ni kazi ambayo:
- Inahatarisha na kuathiri akili, mwili, jamii, au maadili ya watoto. Hii inaweza kujumuisha, kazi katika mashamba makubwa, utumwa au vitendo vinavyofanana na utumwa, ikiwa ni pamoja na uuzaji na usafirishaji haramu wa watoto. Katika maeneo mengine, watoto wanaweza kulazimishwa kujiunga na mizozo ya kivita, kutumika katika utengenezaji na usafirishaji wa madawa ya kulevya, au kuingizwa katika ukahaba. Aina nyingine za ajira ya watoto ni pamoja na kuomba omba, kung’arisha viatu, na kazi za nyumbani.
- Inavuruga masomo yao: kwa kuwanyima watoto fursa ya kuhudhuria shule; kuwalazimisha kuacha shule mapema; au kuwataka kujaribu kuchanganya kuhudhuria shule na kazi nzito kwa muda mrefu.
Ni muhimu kutambua kuwa si kila kazi inayofanywa na watoto inapaswa kuainishwa kama ajira ya watoto. Kwa mfano, shughuli kama kusaidia katika biashara ya familia au kazi za nyumbani kama kuchota maji na kusafisha nje ya saa za shule na wakati wa likizo ya shule huenda hazitachukuliwa kama ajira ya watoto katika nchi nyingi. Hapa Kenya, kwa mfano, Kifungu cha 56 cha Sheria ya Ajira kinasema kuwa mtoto mwenye umri wa kati ya miaka kumi na tatu na kumi na sita anaweza kuajiriwa kufanya kazi nyepesi mradi kazi hiyo haiathiri afya yake, na haimzuii kuhudhuria shule. Shughuli za aina hii zinachangia maendeleo ya watoto na ustawi wa familia zao; zinawapa ujuzi na uzoefu, na kuwasaidia kujiandaa kuwa watu wenye bidii katika jamii siku za usoni.
Madhara ya ajira ya watoto kwa mtoto
Ajira ya watoto inaathiri afya ya mwili na akili ya watoto. Inawanyima haki yao ya kupata elimu bora, inaendeleza umaskini. Inaweza kusababisha ukosefu wa ujuzi na fursa watoto wanapokuwa wazima. Madhara mengine ya ajira ya watoto ni pamoja na:
- Afya ya Mwili na Akili - Watoto wanaoshiriki katika kazi, haswa za aina hatari, mara nyingi wanakabiliwa na hatari za kimwili, kama vile kukabiliwa na kemikali hatari, kazi nzito, na mashine hatari, ambayo yanaweza kusababisha majeraha na hata kifo. Msongo wa mawazo na hali ngumu za kazi zinaweza kuwa na athari mbaya kwa afya ya akili ya watoto, na kusababisha wasiwasi, unyogovu, na trauma.
- Elimu - Ajira ya watoto inavuruga haki ya mtoto ya kupata elimu. Watoto wanaofanya kazi mara nyingi wanauhudhuria shule kwa njia isiyo ya kawaida au wanaacha shule kabisa. Hii inawanyima fursa ya kupata ujuzi na maarifa muhimu kwa ajili ya maisha bora ya baadaye. Katika hali kama hii, watoto hawa wana uwezekano mdogo wa kupata kazi yenye heshima na mapato katika siku zijazo.
- Kutengwa na watoto wengine- Ajira ya watoto inawafanya watoto kutengwa na watoto wengine, ikiwazuia kufurahia utoto wao. Wanakosa fursa ya kuunda urafiki na kuboresha uwezo wao wa kuingiliana na kuwasiliana na watu wengine. Hii inaweza kupelekea hisia za kutengwa na wengine na hisia za kutengwa katika jamii kwa jumla.
- Ukiukwaji wa Haki za Kibinadamu - Ajira ya watoto ni ukiukwaji wa haki za msingi za kibinadamu za watoto. Inawanyima utoto wao, elimu, na fursa ya kufikia uwezo wao wote. Pia ni ukiukwaji wa Shirika la kazi duniani. Nchini Kenya, wazazi, walezi, na waajiri wanaoshiriki katika ajira ya watoto wanaweza kukabiliana na madhara kama ilivyobainishwa katika sheria za Kenya.
Sheria za Kenya kuhusu ajira ya watoto
- Nchini Kenya, kuna sheria zinazolinda watoto kutokana na unyanyasaji na ajira ya watoto. Sheria hizi zinawahusu watu wote wanaoishi au kufanya kazi nchini Kenya. Kulingana na Kifungu cha 53 cha Katiba ya Kenya , kila mtoto ana haki ya kulindwa dhidi ya ukatili, kutelekezwa, desturi hatari, aina zote za ukatili, matendo ya kinyama na adhabu, na ajira hatarishi au za unyanyasaji.
- Kifungu cha 56 cha sheria ya Ajira kinasema kuwa hakuna mtu anayepaswa kumwajiri mtoto ambaye hajaafikia umri wa miaka kumi na tatu, iwe kwa faida au vinginevyo, kwa njia yoyote. Hii ina maana kwamba ajira ya mtoto aliye na umri wa chini ya miaka 13 hairuhusiwi nchini Kenya. Hata hivyo, mtoto mwenye umri wa kati ya miaka kumi na tatu na kumi na sita anaweza kuajiriwa kufanya kazi nyepesi ambayo haitakuwa na madhara kwa afya au maendeleo ya mtoto; na haimzuii mtoto huyu kuhudhuria shule au kushiriki katika programu za mafunzo au kuelekezwa kitaaluma.
- Kifungu cha 53 cha Sheria ya Ajira pia kinakataza aina mbaya za ajira, ambazo Shirika la Kazi Duniani linaelezea kama aina zote za utumwa au vitendo vinavyofanana na utumwa. Hizi ni pamoja na;
-
-
- Kutumia, kupata, au kutoa mtoto kwa ajili ya ukahaba, kwa utengenezaji wa filamu za watu wakubwa (ponografia)
- Kutumia, kupata, au kutoa mtoto kwa ajili ya shughuli haramu, hasa kwa kutengeneza na usafirishaji wa madawa ya kulevya.
-
Sheria hii pia inakataza kuhusisha watoto katika aina yoyote ya kazi inayoweza kuhatarisha afya, usalama, au maadili ya mtoto.
- Kifungu cha 18 cha Sheria ya Watoto kinatoa tamko kwamba: hakuna mtu anayeruhusiwa kumwekea mtoto kazi, utumwa wa nyumbani, unyonyaji wa kiuchumi, au kazi/ajira yoyote ambayo ni hatari, inavuruga elimu ya mtoto, au ina uwezekano wa kuwa na madhara kwa afya ya mtoto au maendeleo yake ya kimwili, kiakili, maadili, au kijamii. Zaidi ya hayo, hakuna mtu anayepaswa kutumia, kupata, au kutoa mtoto kwa ajili ya utumwa au vitendo vinavyofanana na utumwa, ikiwa ni pamoja na:
-
-
- Kuomba omba
- Utumwa wa madeni
- Utumwa, au kazi za kulazimishwa au kazi za lazima au utoaji wa huduma za kibinafsi, iwe kwa faida au la.
-
Nini adhabu ya kumhusisha mtoto katika ajira ya watoto hapa Kenya?
Adhabu: Mtu anayeshiriki katika aina mbaya zaidi za ajira ya watoto au ambaye hafuati kanuni zinazohusiana na ajira ya mtoto anaweza kuadhibiwa kwa faini ya hadi shilingi 200,000 au kifungo cha hadi miezi kumi na mbili au vyote viwili.
Msaada kwa watoto walioathiriwa na ajira ya watoto
Nchini Kenya, Mkurugenzi wa Huduma za Watoto amejiweka katika nafasi ya kutoa msaada kwa watoto ambao haki zao zimekiukwa. Mtu anaweza kuripoti au kutafuta msaada kwa watoto walioathiriwa na ajira ya watoto kwa kuwasiliana na ofisi zao kupitia mawasiliano yaliyopewa hapa chini.
Kuna mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali yanayotoa huduma za ulinzi wa watoto na msaada katika kambi za wakimbizi za Kakuma, Kalobeyei, na Dadaab. Unaweza kuwasiliana na mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali kupitia mawasiliano yafuatayo:
Shirika la kuwakinga watoto | Taarifa la mawasiliano |
Directorate of Children Services (DCS) |
National Child Helplines
DSS contacts
|
Save the Children (SCI) |
Dadaab
|
Terre Des Hommes (Tdh)
|
Dadaab:
Kalobeyei
|
Danish Refugee Council (DRC) |
Kakuma/Kalobeyei
Nairobi
|
Kwa maelezo zaidi kuhusu huduma za watoto zinazotolewa na mashirika katika Kakuma na Dadaab, angalia hapa chini:
- Terre des Hommes (TdH) (Kalobeyei) - Case Management
- Refugee Consortium of Kenya (RCK) – Children Services
- Humanity and Inclusion (HI) - Child Protection Services
- Department of Children Services – Shelter
- Save the Children International (SCI) IFO 2 – Psychosocial Support
- Save the Children International (SCI) IFO 2 –Social Services
- Save the Children International (SCI) IFO 2 – Education Services
Ikiwa una maswali yoyote, tafadhali tuandikie kupitia ukurasa wa Facebook wa Julisha.Info au zungumza nasi kupitia WhatsApp (+254110601820) ,Jumatatu hadi Ijumaa kutoka 08:00 asubuhi hadi 5:00 jioni