Hazina ya Kitaifa ya Ustawi wa Jamii (NSSF) ulizindua mpango wa akiba wa Haba Haba tarehe 30 Oktoba 2024 ili kuwajumuisha watu walio kwenye sekta isiyo rasmi. Sekta isiyo rasmi inajumuisha biashara ndogo ndogo zinazoendeshwa na watu ambao wanapata kipato lakini hawajumuishwi kwenye mikato ya lazima ya serikali. Mpango wa Akiba wa Haba Haba unasimamiwa na Hazina ya Kitaifa Ya Ustawi wa Jamii (NSSF), taasisi ya serikali chini ya Wizara ya Leba na Ulinzi wa Jamii.
Tumeandaa maswali yanayoulizwa mara kwa mara na majibu yake ili upate taarifa kamili na ufahamu faida zote zinazotolewa.
Haba Haba ni Nini?
Haba Haba ni mpango wa akiba uliobuniwa kwa ajili ya watu wanaofanya kazi kwenye sekta isiyo rasmi. Mpango huu wa hifadhi ya jamii unasimamiwa na Hazina ya Kitaifa Ya Ustawi wa Jamii (NSSF), taasisi ya serikali chini ya Wizara ya Leba na Ulinzi wa Jamii.
Nani Anaweza Kujiunga na Haba Haba?
Mkenya yeyote au mkimbizi mwenye umri wa miaka 18 au zaidi na mwenye kitambulisho halali cha taifa au kitambulisho cha ukimbizi. Ikiwa huna kitambulisho halali cha ukimbizi, tembelea ofisi ya karibu ya Idara ya Huduma za Wakimbizi (DRS) ili kuomba au kusasisha kitambulisho chako. Hakuna kikomo cha juu cha umri wa kujiunga na mpango wa Haba Haba.
Baadhi ya Faida za Kiuchumi za Kujiunga na Mpango wa Akiba wa NSSF Haba Haba
Ili kupata faida za mpango wa akiba wa NSSF Haba Haba, utahitaji kuwa na nambari ya M-Pesa halali au akaunti ya benki iliyosajiliwa kwa jina lako. Tafadhali tembelea kituo chochote cha Huduma Center au ofisi ya NSSF iliyo karibu ukiwa na kitambulisho chako cha taifa au cha ukimbizi pamoja na kadi ya NSSF ili kuomba kutoa akiba yako.
- Faida za Kutoa Akiba na Kustaafu: Unaweza kutoa 50% ya akiba yako baada ya kuchangia mfululizo kwa miaka 5 na angalau Ksh 4,800 kwa mwaka. Unaweza kutoa 50% iliyobaki kama malipo ya mara moja unapofikisha umri wa miaka 50 au zaidi. Mahitaji: Kadi ya NSSF, kitambulisho cha taifa/cha ukimbizi.
- Faida kwa Watu Wenye Ulemavu: Unaweza kupokea akiba yako yote ikiwa umepata ulemavu wa kudumu kutokana na ugonjwa au ajali. Mahitaji: Kadi ya NSSF, kitambulisho cha taifa/cha ukimbizi, cheti cha bodi ya matibabu.
- Faida kwa Waliohamia Nje ya Nchi: Pokea akiba yako yote unapohamia nje ya Kenya kwa kudumu. Mahitaji: Kadi ya NSSF, kitambulisho cha ukimbizi, hati ya kutoka iliyotolewa na DRS na Fomu ya Ombi la Kurudi Nyumbani (VRF) kutoka UNHCR na iliyothibitishwa na ofisi ya uhamiaji.
- Faida kwa Wategemezi: Iwapo mwanachama atafariki, kiasi chote cha akiba kitalipwa kwa wategemezi wake, kwa kuzingatia kwanza mwenzi/mwenza na watoto, wazazi, ndugu, au mlezi. Mahitaji: Ushahidi wa kifo, uthibitisho wa uhusiano, kitambulisho cha mlalamikaji.
Jinsi ya Kujiandikisha kwa Mpango wa Akiba wa NSSF Haba Haba kama Mkimbizi Kenya
Kuna njia mbili za kujiandikisha kwenye mpango wa NSSF Haba Haba. Chaguo hizi mbili pia zinaweza kutumiwa na Wakenya wanaotaka kuwa sehemu ya mpango wa akiba wa kustaafu wa Haba Haba.
- Usajili wa Ana kwa Ana: Tembelea kituo cha Huduma au ofisi ya karibu ya NSSF ili kusaidiwa kujiandikisha. Utahitaji kuwa na kitambulisho cha ukimbizi au cha taifa na mchango wa Ksh 200.
- Usajili kwa Simu: Piga *303# kwenye simu yako na fuata maelekezo. Mchango wa Ksh 200 na kitambulisho vinahitajika wakati wa usajili. Ikiwa kuna mabadiliko katika taarifa zako binafsi au jina la mrithi wako, tembelea ofisi ya karibu ya NSSF ukiwa na ushahidi na barua kutoka DRS ili taarifa zako zisasishwe.
Je, Ikiwa Tayari Nimejiandikisha na NSSF?
Ikiwa tayari umejiandikisha na NSSF au Haba Haba, HAKUNA haja ya kujiandikisha tena. Ikiwa umepoteza kadi yako ya NSSF, tembelea ofisi yoyote ya NSSF iliyo karibu ukiwa na kitambulisho chako ili kuomba kadi mpya. Ada ya Ksh 200 itatozwa kwa kadi mpya.
Mahitaji ya Akiba na Michango
Michango ya chini: Ksh 400 kwa mwezi. Vinginevyo, unaweza kulipa Ksh 25 kwa siku. Hakikisha unachangia angalau Ksh 400 kila mwezi ili kufuzu kwa kutoa akiba ya muda mfupi baada ya miaka 5. Hakuna adhabu kwa kukosa malipo ya chini, lakini kama hutalipa angalau Ksh 400 kwa mwezi au Ksh 4,800 kwa mwaka, hutaweza kutoa akiba ya muda mfupi baada ya miaka 5.
Jinsi ya Kulipia Akaunti Yako ya NSSF Haba Haba
Kulipa kwa M-Pesa
- Ingiza Paybill Number: 222222
- Weka NSSFV- ikifuatiwa na nambari yako ya NSSF, kama ifuatavyo: NSSFV-123456789
- Weka kiasi na PIN yako unapoombwa na ukamilishe malipo.
- Utapokea ujumbe wa kuthibitisha malipo.
Kulipa Mtandaoni
- Bonyeza kiungo cha huduma ya kidijitali ya NSSF: https://nssfdigital.enssf.co.ke/home.
- Bonyeza “Self Service” na chagua “Voluntary Contribution.”
- Ingiza nambari yako ya mwanachama ya NSSF, thibitisha na fuata hatua zilizopo.
Jinsi ya Kuangalia na Kufuatilia Akiba Yako ya NSSF Haba Haba
Ili kuangalia akiba yako, piga *303# na fuata maelekezo au tembelea kituo chochote cha Huduma au ofisi ya NSSF iliyo karibu kwa msaada kuhusu salio la akaunti yako ya Haba Haba.
Jinsi ya Kulipwa na Haba Haba
Utalipwa jumla ya akiba yako pamoja na riba iliyopatikana (mapato ya uwekezaji yanatangazwa na NSSF). Pesa zitalipwa kupitia M-Pesa kwa nambari yako ya simu iliyosajiliwa au moja kwa moja kwenye akaunti yako ya benki.
Habari za Mawasiliano
Kwa maswali, unaweza kufika kwa Idara ya Huduma za Wakimbizi na NSSF kupitia mawasiliano yafuatayo:
NSSF Line ya bure: 0800 221 2744 Simu: 0704 303 303 Tovuti: www.nssf.or.ke Barua pepe: info@nssfkenya.co.ke Tembelea Kituo cha Huduma cha karibu au ofisi ya NSSF Piga simu kwa namba ya msaada ya UNHCR: 1517 |
Kwa taarifa kuhusu ofisi ya DRS: Simu: (020) 4405057 |
Ikiwa una maswali yoyote, tafadhali tuandikie kupitia ukurasa wa Facebook wa Julisha.Info au zungumza nasi kupitia WhatsApp (+254110601820) ,Jumatatu hadi Ijumaa kutoka 08:00 asubuhi hadi 5:00 jioni