Jambo la Kuzingatia: Mnamo Oktoba 2022, serikali ya Kenya iliteua jopokazi la kukusanya maoni ya umma kuhusu utekelezaji wa Mtaala unaozingatia Umahiri (CBC) na kutoa mapendekezo. Ukusanyaji wa maoni ya umma ulihitimishwa mnamo Novemba 2022. Kwa sasa serikali inapitia matokeo ya jopokazi hilo. Mara tu mchakato huu utakapokamilika, tutasasisha makala haya ili kujumuisha mabadiliko yatakayofanywa kwenye mtaala.
Je, unataka kujua kuhusu mahitaji, masomo, mafunzo na mchakato wa mitihani ya elimu ya msingi ya juu?
Mfumo wa elimu wa Kenya ulipitia mabadiliko makubwa huku kukianzishwa mtaala unaozingatia umahiri (CBC) mnamo Desemba 2017. Mabadiliko haya yalijumuisha marekebisho katika mada, mikabala ya mitihani, na kuanzishwa kwa viwango vipya.
Kiwango cha elimu ya msingi ya juu, ambayo inajumuisha darasa la 4, 5, na 6, inalenga wanafunzi wenye umri wa kati ya miaka 9 na 11 ambao wamemaliza elimu ya msingi ya chini. Mtihani wa kitaifa unafanya mwishoni mwa gredi 6 ili kupima ujuzi wa wanafunzi katika masomo yanayofundishwa katika hatua hii.
Maelezo zaidi kuhusu hatua nyingine ya CBC ni:
- Masomo ya CBC nchini Kenya kwa wanafunzi wa PP1 na PP2
- Mtaala wa CBC nchini Kenya: Unayostahili kujua kuhusu elimu ya msingi - gredi ya kwanza, pili na ya tatu
- Mchakato wa uteuzi wa shule za sekondari za upeo wa chini, masomo na elimu nchini Kenya
- Secondary education
- Tertiary level education
Masomo na mafunzo ya Gredi ya 4, 5 na 6 chini ya mfumo wa masomo wa Kenya wa CBC
- Masomo angalau 10 lazima yafundishwe katika kiwango cha elimu ya msingi ya juu
- Wanafunzi wanatarajiwa kuchagua somo moja ya lugh ya kigeni kama somo la ziada. Hii inaweza kuwa Kiarabu, Kijerumani, Kifaranza ama Kichina (Mandarin)
- Somo la lugha ya kigeni litafunzwa mara mbili kwa wiki.
- Ujuzi wa Teknolojia ya Mawasiliano ya Habari (TEHAMA ama ICT) pia hufundishwa katika kila somo.
- Walimu pia huhakikisha kuwa wanafunzi wanajifunza stadi za msingi za maisha na uzoefu mwingine wa maisha halisi.
Masomo ambayo lazima yasomwe katika Gredi 4, 5 na 6 kila wiki ni:
- Masomo manne ya Kiingereza
- Masomo manne ya Kiswahili ama Lugha ya Alama ya Kenya (KSL) kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia
- Masomo matatu ya Sayansi kimu (Home Science)
- Masomo matatu ya Kilimo
- Masomo manne ya Sayansi na Teknolojia
- Masomo matano ya hisabati
- Masomo matatu ya Elimu ya Dini - Elimu ya Dini ya Kikristo, Kiislamu au Kihindu
- Masomo matatu ya Sanaa ya Ubunifu (Creative Arts)
- Masomo matano ya Elimu ya Kimwili na Afya
- Masomo matatu ya Maarifa ya Jamii
Wanafunzi pia watashiriki katika maelekezo ya programu ya kichungaji (PPI) mara moja kwa wiki ili kujifunza na kutekeleza imani, tabia na ustawi wao wa kihisia kwa msaada wa taasisi za kidini na viongozi.
Wanafunzi wenye ulemavu wa kimwili kwa kawaida hujumuishwa katika madarasa ya kawaida. Wanafunzi wenye ulemavu wa kuona na kusikia wanafundishwa na walimu wa Elimu ya Mahitaji Maalum (SNE) katika shule maalum na masomo yao hutafsiriwa kwa maandishi ya vipofu (braille) na Lugha ya Ishara ya Kenya (KSL).
Vifaa vya CBC vya kujifunzia kwa wanafunzi wa gredi 4, 5 na 6.
Wanafunzi wa elimu ya msingi ya juuwatatambulishwa kwa vifaa tofauti huku wakihudhuria masomo tofauti. Hii husaidia wanafunzi kupata maarifa ya vitendo kuhusu masomo wanayosoma.
- Kilimo
Ili kujifunza somo la kilimo kwa vitendo, walimu watatumia vifaa kulingana na mahitaji ya somo hilo. Vifaa ambavyo wanafunzi watatumia ni kama vile nyundo, koleo(pliers), kisu, mwiko wa bustani, panga, jembe, upanga (slasher), sepeto (spade), kolego, toroli, uma wa samadi, uma jembe, kipimo cha mkanda, kamba, msumeno wa kupogoa na chombo cha kunyunyiza maji ni vifaa vya kawaida vinavyotumika kujifunza kilimo.
- Sanaa ya Ubunifu
Wanafunzi watajifunza jinsi ya kuthamini ubunifu wao na kufanya mazoezi ili kufaulu katika maeneo kama kuchonga, kazi ya ngozi, muundo wa kiasili na kidijitali, uwekaji alama wa picha na ufundi. Vifaa vingi watakavyotumia ni vya kawaida na vinapatikana kama; ngozi iliyotumika, gundi, sindano, nyuzi, shanga, karatasi, penseli, vitabu vya kuchora, mbao, zana za kukata ngozi, sampuli za nakshi, vinyago, na vifaa vya kutoboa na kupachika.
- Sayansi kimu
Somo hili linaangazia jinsi ya kuandaa na kula vyakula vyenye afya, kuepuka kupata magonjwa, faraja ya jumla, na usalama nyumbani, kutunza usafi wa kibinafsi, kupanga bajeti na kununua vitu. Wanafunzi watajifunza kwa kutazama video, kutazama picha, au kutumia zana halisi kama vile vyungu vya kupikia vilivyoboreshwa, vifaa vya kufulia, vikombe vya kupimia, vijiko, visu, pini za kubingiria, majiko ya mkaa, vifaa vya kushona na kufuma,nyuzi za kushona kati ya vitu vingine. Wanafunzi pia wanatarajiwa kuunda vilabu vya sayansi kimu shuleni kwa ajili ya kujifunza kwa kushirikiana na wanafunzi wenzao.
- Sayansi na Teknolojia
Wanafunzi hujifunza kuhusu mazingira, mimea na wanyama kwenye somo hili. Pia wanajifunza kuhusu afya ya uzazi na jinsia ya binadamu. Wanafunzi pia watajifunza taaluma ya kompyuta, kwa mfano, kuandaa lahadata kwa kutumia Microsoft excel
Mtihani wa Taifa wa CBC kwa wanafunzi wa gredi ya sita
Tathmini ya Elimu ya Shule ya Msingi ya Kenya (KPSEA) ya kwanza kabisa ilifanyika mnamo Novemba 2022. KPSEA imeundwa kutathmini uwezo wa kila mwanafunzi katika gredi ya sita, ambao ni mwaka wa mwisho katika shule ya msingi ya juu, kabla ya kuendelea na elimu ya shule ya upili ya upeo wa chini.
Wanafunzi hufanya mitihani minne katika muda wa siku tatu. Mitihani hiyo ni Hisabati, Kiingereza, Kiswahili, na Sayansi Jumuishi. Sayansi kimu, kilimo, sayansi na teknolojia, na afya zote zinatathminiwa kama Sayansi Jumuishi
Wanafunzi wanaohitaji maandishi ya vipofu, maandishi makubwa na Lugha ya Ishara ya Kenya wanaweza pia kufanya majaribio huku kukiwa na mabadiliko fulani katika muda wa kufanya mitihani yao. Mabadiliko hayo ni:
- Mtihani wa Hisabati na Hisabati (maandishi makubwa) huchukua saa moja na dakika 20, wakati Hisabati (maandishi ya vipofu) huchukua saa moja na dakika 50.
- Mtihani wa Kiingereza na Kiingereza (maandishi makubwa) huchukua saa moja, huku Kiingereza (KSL), na Kiingereza (maandishi ya vipofu) huchukua saa moja na dakika 20.
- Mtihani wa Kiswahili na KSL inachukua saa moja na Kiswahili (maandishi ya vipofu) huchukua saa moja na dakika 20.
- Mtihani wa Sayansi Jumuishi huchukua saa moja na dakika 40, na mitihani ya Sayansi Jumuishi (maandishi makubwa) na Sayansi Jumuishi (maandishi ya vipofu) huchukua saa mbili na dakika 10.
Mara tu matokeo yatakapotangazwa na wizara ya elimu, wazazi na walezi wanaweza kupata matokeo ya KPSEA kutoka kwa shule walizosomea wanafunzi. Wanafunzi wote wanaweza kuendelea na shule za sekondari za chini bila kuzingatia kama matokeo ya mitihani yao ya elimu ya msingi ya juu.
Unaweza kupata taarifa zaidi kuhusu mfumo wa elimu wa CBC nchini Kenya CBC kupitia tovuti ya Taasisi ya Kukuza Mitaala ya Kenya (KICD).
Ikiwa una maswali yoyote, tafadhali tuandikie kupitia ukurasa wa Facebook wa Julisha.Info au zungumza nasi kupitia WhatsApp (+254110601820) ,Jumatatu hadi Ijumaa kutoka 08:00 asubuhi hadi 5:00 jioni