Divorce_Document_Images_.png

Watu wawili wakifunga ndoa, wanatarajia kuwa pamoja kwa maisha yao yote. Hata hivyo, maisha huwa hayaendi kama ilivyopangwa kila wakati na wakati mwingine huenda wawili hao wakaamua kutengana kwa sababu moja au nyingine.

Kama ilivyojadiliwa katika nakala hii, Sheria ya Ndoa nchini Kenya inatambua mifumo 5 ya ndoa – Ndoa ya Kiraia, ya Kikristo, ya Kihindu, ya Kimila na ya Kiislamu. Vivyo hivyo, Sheria ya Ndoa inaelezea jinsi aina hizi tofauti za ndoa zinapaswa kufutwa.

Hapa chini, tutaangalia

Mfumo wa kutoa talaka nchini Kenya huangalia ni nani ana kosa. Hii inamaanisha kuwa sheria inaruhusu kuvunjika kwa ndoa ikiwa mtu anayetaka talaka atathibitisha kuwa mwenzake alifanya kosa la ndoa.

Katika nakala hii, tutaangazia mazingira tofauti ambayo talaka hutolewa nchini Kenya:

Sababu za talaka katika ndoa za Kikristo, za Kiraia na za Kimila

Sababu za kawaida za talaka kutolewa katika ndoa za Kikristo, za Kiraia na za Kimila nchini Kenya ni:

  1. Vitendo vya uzinzi vinavyofanywa na wanandoa.
  2. Ukatili, iwe kiakili au kimwili, unaosababishwa na mwanandoa kwa mwenzake au kwa watoto wao
  3. Kutelekezwa kwa angalau miaka mitatu (3) kabla ya tarehe wanapowasilisha ombi lao la talaka
  4. Ufisadi wa kipekee wa kimaadili au uovu.
  5. Kuvunjika kabisa kwa ndoa.

Kulingana na sheria za Kenya, ndoa huwa imevunjika kabisa wakati:

  • Mmoja wa wanandoa akizini
  • Mmoja wa wanandoa akiwa mkatili kwa mwenzake au kwa mtoto yeyote aliyezaliwa katika ndoa hiyo.
  • Mmoja wa wanandoa akimpuuza mwenzake kimaksudi kwa anagalau miaka miwili.
  • Wanandoa wakitengana kwa angalau miaka miwili
  • Mmoja wa wanandoa akimuacha mwenzake kwa angalau miaka mitatu.
  • Mmoja wa wanandoa akihukumiwa kifungo cha maisha jela au kwa kipindi cha miaka saba au zaidi.
  • Mmoja wa wanandoa akipatikana na shida kali ya afya ya akili - Hii inapaswa kudhibitishwa na madaktari wawili na mmoja wao lazima awe daktari wa magonjwa ya akili.

Sababu zaidi za talaka kuruhusiwa katika ndoa za kisheria.

Watu waliooana katika ndoa ya kisheria hawawezi kuitisha korti iwtenganishe ama iwape talaka ikiwa wameona kwa muda usizidi mika mitatu (3).

Korti inaweza unaweza kutuma kesi ya ndoa ya kiraia kwa mchakato wa upatanisho uliokubaliwa na wanandoa. Usuluhishi ulioambatanishwa na korti ni mchakato wa hiari na unatambuliwa na mfumo wa mahakama. Hii inamaanisha kwamba mara tu korti inapowasilisha mzozo huo kwa mchakato wa upatanishi na wanandoa hao kukubali, wanatarajiwa kurudi kortini baada ya siku 60 na ripoti kutoka kwa mpatanishi. Baada ya usuluhishi, wanandoa hao wanaweza kuchagua kusuluhisha mambo au kuendelea na kutafuta talaka.

Sababu zaidi za talaka kuruhusiwa katika ndoa za kitamaduni.

  • Sababu za nyongeza za talaka chini ya ndoa ya kitamaduni zinaweza kujumuisha sababu zingine zozote chini ya mila ya jamii ambayo wanandoa walifunga ndoa yao. Kwa mfano ikiwa mtu huyo amekamatwa akifanya uhalifu kama vile wizi, hii inaweza kuwa sababu ya kupata talaka kwani tamaduni zingine zinaamini kuwa tabia hii inaweza kuwa katika familia na watoto waliopatikana kutoka kwa ndoa hiyo watakuwa wahalifu.
  • Wanandoa walioolewa chini ya ndoa ya kitamaduni wanaweza kupitia mchakato wa upatanisho au utatuzi wa mizozo ya kimila kabla ya mahakama kutoa uamuzi kuhusu ombi lao la talaka. Katika jamii nyingi, wazee watajaribu kuwapatanisha wawili hao kabla ya talaka kutolewa. Walakini, ikiwa watashindwa, wazee watapeana ridhaa ya kuvunja ndoa.
  • Mtu atakaye wafanyisha wenzi mchakato wa utatuzi wa migogoro ataandaa ripoti ya mchakato huo kwa korti.

Talaka katika ndoa za Kihindu.

Mtu aliyeolewa katika ndoa ya Kihindu anaweza kuitisha korti talaka ikiwa:

  1. Ndoa hiyo imevunjika kabisa.
  2. Mwenzake amemuacha kwa angalau miaka mitatu (3).
  3. Mwenzake amebadili dini.
  4. Mwenzake amefanya makosa ya ubakaji, kulawiti, kulala na mnyama, au kuzini katika kipindi ambacho wameona.
  5. Mwenzake amekuwa mkatili kwake.
  6. Mwenzake amemfanyia ufisadi wa kipekee.

Talaka katika ndoa za Kiislamu

Talaka katika ndoa za Kiislamu zinasimamiwa na sheria za Kiislamu. Wanandoa waliofunga ndoa za kiislamu wanaweza kutembelea Korti ya Kadhi  ambapo watashauriwa kuhusu taratibu za talaka.

Baadhi ya sababu za kutolewa talaka katika ndoa za kiislamu ni pamoja na:

  1. Uzinzi au utovu wa uaminifu
  2. Aina yoyote ya fujo - kuumizwa kimwili, kifedha, au kihisia na mwenzako
  3. Pale mwenzi anapopatwa na kasoro fulani za kimwili, kama ukosefu wa nguvu za kizazi.
  4. Pale ambapo wanandoa wanakuwa na tofauti za kidini

Wakati Kadhi, sheikh, imamu au mtu mwingine aliyeidhinishwa na Msajili wa ndoa akiwapatia wanandoa walioolewa chini ya ndoa ya Kiislamu talaka, anapaswa kupeleka nakala ya agizo la talaka kwa Msajili wa Ndoa.

Mchakato wa talaka

Hatua ya 1: Kuwasilisha Ombi

Mchakato wa talaka huanza wakati mtu anayetaka talaka (mwombaji) anapowasilisha ombi la talaka kortini. Katika ombi hilo wataelezea kwa nini wanataka talaka, na ombi hilo pia litakuwa na:

  • Hati ya Kudhibitisha - tamko lililoapishwa na mwombaji akisema kuwa yaliyomo kwenye ombi ni kweli kwa kadiri ya ujuzi wao, habari, na imani.
  • Ilani ya Kuonekana- hati inayomtahadharisha mlalamikiwa kwamba ombi limewasilishwa dhidi yao.
  • Kukubali Ombi- hati iliyosainiwa na mhojiwa kibinafsi kukiri kwamba wamepokea ombi.
  • Orodha ya Mashahidi - Orodha ya mashahidi ambao mwombaji amekusudia kuwita ili watoe ushahidi wakati wa kusikilizwa kwa ombi.
  • Taarifa za Mashahidi - Mashahidi lazima watoe taarifa zao zilizotiwa saini (akaunti ya ukweli kama ilivyosemwa na mwombaji)
  • Orodha ya Nyaraka - Ikiwa unataka kutegemea nyaraka, lazima utoe orodha yao na uambatishe nakala kwenye ombi.

Hatua ya 2: Ilani ya kuonekana

Baada ya mwombaji kuwasilisha ombi hilo, hakimu atatia saini Ilani ya Kuonekana. Hii ni hati inayomtahadharisha Mdaiwa (upande mwingine) kuwa ombi/kesi limewasilishwa dhidi yao na kwamba wanapaswa kujibu (toa taarifa rasmi kwamba wao au wakili wao wanapanga kudumisha au kupinga suala hilo) kabla ya siku kumi na tano (15) kuisha.

 

Hatua ya 3: Jibu la Mlalamikiwa

Ikiwa mlalamikiwa atapinga ombi la talaka, atalazimika kutoa jibu na kumtumia Mwombaji.

 

Hatua ya 4: Cheti cha Msajili

Baada ya siku 15, Mwombaji atauliza korti itoe Cheti cha Msajili. Hii inamaanisha kuwa ombi liko tayari kwenda kusikilizwa kortini

 

Hatua ya 5:  Kusikizwa kwa Ombi

Siku ya kusikilizwa kwa ombi limeamuliwa. Wakati wa kusikilizwa kwa Ombi, Mwombaji ataleta ushahidi kuonyesha korti kuwa ndoa hiyo imevunjika. Ikiwa Mtuhumiwa atapinga ombi hilo, atatakiwa pia kuwa na mashahidi na kuleta ushahidi wa kuunga mkono kesi yake.

Mara tu hii itakapofanyika, korti itaweka tarehe ya uamuzi.

 

Hatua ya 6: Decree Nisii

Siku ya kutolewa kwa uamuzi, korti itaamua ikiwa kuna sababu za kutosha za talaka kutolewa. Ikiwa itapata sababu za kutosha, itatoa amri ya kwanza ya talaka, inayojulikana kama Decree Nisii.

Wanandoa sasa watakuwa na mwezi wa kuamua ikiwa wanataka talaka ipitishwe au la. Mara tu amri ya Decree Nisii ikitolewa, utakuwa na mwezi 1 kuamua ikiwa kweli unataka ndoa ivunjwe rasmi au la. 

Hatua ya 7: Decree Absolute

Baada ya mwezi mmoja kumalizika na hakujakuwa na mabadiliko yoyote, korti sasa itatoa amri ijulikanayo kama Decree Absolute.

Hii ni hatua ya mwisho ya mchakato wa talaka na inathibitisha kwamba ndoa hiyo imefutwa.

 

Wakimbizi na wanaotafuta hifadhi nchini Kenya wanahimizwa kutafuta ushauri wa kisheria kuhusu maswala ya talaka kwa sababu mchakato huo unaweza kuwa mgumu.

Kwa ushauri wa kisheria kuhusu talaka, unaweza kuwasiliana na:

Nairobi

Refugee Consortium of Kenya (RCK)

  1. Piga simu kwa nambari +254733860669 ama +254720943164
  2. Tembelea Ofisi za RCK zinazopatikana katika Nyumba ya Haki House katika barabara ya Ndemi, karibu na barabara ya Muringa sehemu ya Kilimani, Nairobi.

Ofisi za RCK zinafunguliwa kutoka saa 2 asubuhi hadi saa 11 jini kila Jumatatu hadi Ijumaa.

 

Kakuma

Refugee Consortium of Kenya (RCK)

Piga simu kwa nambari - 0800720262 na 0701414978 ama utembelee ofisi za RCK

Huduma zinatolewa Jumatatau hadi Alhamisi katika ofisi za RCK zinazopatikana LWF compound.

Huduma hizo pia hutolewa Alhamisi katika ofisi za RCK zinazopatikana sehemu ya Kakuma 4, mkabala na Kituo cha polisi cha Kakuma 4.

 

Dadaab:

Refugee Consortioum of Kenya (RCK)

Tembelea ofisi za RCK katika kambi ya wakimbizi ya Hagadera.

Ofisi hizo zinatoa huduma kutoka saa 2 hadi saa 11 jumatatu hadi Ijumaa.

 

Je, unatafuta ushauri na usaidizi wa kisheria bila malipo katika kusajili ndoa au talaka? Unaweza kuwasiliana na shirika la Kituo Cha Sheria kwa usaidizi. 

Kituo Cha Sheria ni shirika la usaidizi wa kisheria nchini Kenya ambalo hutoa huduma za kisheria bila malipo kwa wale ambao hawawezi kumudu. Shirika hilo lina afisi Nairobi, Mombasa, na afisi ya tawi katika eneo la Pangani, Nairobi, kutoa usaidizi wa kisheria kwa watu binafsi na jamii kote nchini. 

Ofisi kuu 

Ofisi kuu ya Kituo Cha Sheria iko kwenye makutano ya barabara ya Ole Odume na barabara ya Argwings Kodhek, mkabala na tume kuu ya Bangladesh. Unaweza kuwasiliana na makao makuu kwa kupiga simu 0734 874221 au 0727 773991 au kwa barua pepe info@kituochasheria.or.ke 

Ofisi ya Mombasa 

Kwa wale wanaoishi Mombasa, Kituo cha Ofisi ya Mkoa wa Pwani iko kwenye Mtaa wa Taratibu huko Tudor, karibu na chuo kikuu cha kiufundi cha Mombasa na karibu na Hoteli ya White Rhino. Unaweza kufikia timu kwa kupiga simu 0731 129739 au 0700 638379, au kwa barua pepe msa@kituochasheria.or.ke 

Ofisi ya Pangani 

Kituo Cha Sheria pia wana ofisi ya tawi katika eneo la Pangani la Nairobi, iliyoko KCDF House, ghorofa ya 4, Barabara ya Chai/Pamba, nje ya Barabara ya Juja. Ofisi ya tawi ya Pangani inaweza kupatikana kwa kupiga simu 0736 867241 au 0720 806531, au kwa barua pepe fmp@kituochasheria.or.ke 

Unaweza pia kutuma hoja yako ya kisheria kama ujumbe mfupi wa maandishi kwa Kiingereza au Kiswahili kwa 0700777333 na usubiri jibu kutoka kwa wataalamu wa sheria wa Kituo. 

 

Je, una swali lolote linalohusiana na nakala hii? Wasiliana nasi kupitia ukurasa wa Facebook wa Julisha.Info, Jumatatu hadi Ijumaa kutoka saa 2 asubuhi hadi saa 11 jioni.