mceclip0.png

Ali Omar mwenye umri wa miaka 27 anatengeneza kiti cha magurudumu kinachoweza kubadilishwa katika Kituo cha Ukarabati cha Jamii kinachoendeshwa na Shirika la Ulimwengu la Kilutheri (LWF) huko Hagadera, Kambi ya Wakimbizi ya Dadaab. PICHA: Julisha.Info]

Je! Unajua kwamba karibu watu bilioni 1.18 wanaishi na ulemavu ulimwenguni? Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), karibu asilimia 15 ya idadi ya watu ulimwenguni wanapitia aina fulani ya ulemavu. Idadi hii inakaribia kuwa sawa na idadi ya raia wa India, nchi ya pili duniani kwenye orodha ya nchi zenye idadi kubwa zaidi ya watu.

Licha ya kuwa kawaida sana, katika mazingira mengine, ulemavu bado unaonekana kama mwiko, laana au mzigo. Hali sio tofauti katika mazingira ya kambi ya wakimbizi. Watu wenye Ulemavu (PWDs) wanabaki katika hatari ya kukabiliwa na unyanyasaji wa mwili na kisaikolojia kwa sababu ya kutojua, umaskini, na ukosefu wa ufahamu kuhusu ulemavu kati ya wakimbizi na jamii zinazotoa hifadhi kwa wakimbizi.

Huko Dadaab, Noor Ibrahim, mwenye umri wa miaka 29 na Ali Omar  mwenye umri wa miaka 27 walichagua kuleta mabadiliko. Wawili hao hawajafanya kazi nyingine maishani mwao yote ila kuwahudumia wakimbizi wanaoishi na ulemavu. Noor anasema ataadhimisha Siku ya Kimataifa ya Vijana mwaka huu kama hafla maalum kwake kusherehekea miaka yake 13 ya kuwatumikia wanaoishi na ulemavu. Yeye ni msimamizi wa mafundi katika Kituo cha Ukarabati cha Jamii kinachoendeshwa na Shirika la Ulimwengu la Kilutheri (LWF) huko Hagadera.

“Nimejifunza mengi kuhusu aina mbali mbali za ulemavu na aina ya msaada unaohitajika. Hakuna mtu anayeweza kuepuka ulemavu. Sisi sote tunahitaji kuwa na ujuzi huu. Ulemavu unaweza kutokea wakati wowote, kwako au kwa mtu wa karibu sana kwako. Ulemavu sio mwiko au laana,” anafafanua Noor.

mceclip1.png

 [Noor Ibrahim, Msimamizi wa mafundi wa LWF akirekebisha kiti cha magurudumu katika Kituo cha Ukarabati cha Jamii huko Hagadera, Dadaab. PICHA: Julisha.info]

Noor na Ali hufanya kazi ya mikono. Baada ya kutolewa kwa vifaa vinavyosaidia kusonga kwa wanaoishi na ulemavu katika kambi, wanapewa jukumu la kuwafunza wateja wao kuhusu matumizi, ukarabati na matengenezo ya vifaa hivyo. Kinachofurahisha zaidi ni jinsi wanavyofanya kazi kwa pamoja. Wawili hawa wamefunzwa kukarabati na kutengeneza viti vya magurudumu vilivyotengenezwa kufuatia mahitaji maalum ya watumizi wao, viti vya choo, na hata vifaa vya kuwasaidia watoto wanaoishi na ulemavu wa kupooza kwa ubongo (cerebral palsy) kuweza kuketi na kusimama.

Ali anaelezea kuwa watu wanaotumia viti vya magurudumu vyenye mzunguko wa mafurudumu tatu bado wanakabiliwa na changamoto za kuweza kusonga  kambini. Eneo hilo lina mchanga mwingi na kama vile viti vya magurudumu vilivyosaidiwa - kwa wazee na watoto watoto wanaoishi na ulemavu wa kupooza kwa ubongo (cerebral palsy), watumizi wengi hawawezi kuzunguka kutoka sehemu moja kwenda nyingine bila msaada. Ali anataka vijana zaidi kukumbatia na kukuza utamaduni wa kusaidia wale ambao wanahitaji kusukumwa kwenye viti vya magurudumu.

"Tunatoa pampu, spana za magurudumu na tunawasaidia kujifunza jinsi ya kurekebisha pancha na kukabiliana na changamoto zingine kawaida za kiufundi. Licha ya msaada huu, kambini mchanga hufanya harakati za mzunguko wa magurudumu matatu kuwa changamoto. Watumizi wengi wa vifaa hivu huhitaji kusukumwa ili kuweza kupata huduma kwenye kambi. Tunapaswa kuwa tayari kusaidia kila wakati,” aliomba Ali.

Amina (sio jina lake halisi), mama wa watoto 7, ni mmoja wa wateja wao. Alipata ugonjwa ambao ulimlazimisha kuhitaji msaada kamili kutoka kwa wanawe wawili tangu Juni 2020. Hakuweza kusimama peke yake. Hii ilimaanisha kuwa alikabiliwa na changamoto katika kupata huduma za msingi kama vile huduma ya afya ambayo hutolewa bure kwa wakimbizi na wanaotafuta hifadhi kambini.

Ilikuwa hadi Machi 2021 ambapo wanawe, kupitia msaada wa viongozi wa jamii, walimpeleka katika kituo cha Ukarabati cha Jamii cha LWF ambapo Noor na Ali wanahudumu.

Katika kituo cha Ukarabati huko Hagadera, Amina alifanyiwa tibamaungo (Physiothraphy) na kupewa vifaa vya bure vya kusaidia. Sasa anaweza kutembea mwenyewe baada ya vipindi kadhaa vya tibamaungo.

“Nilianza na tibamaungo na baada ya mwezi mmoja, niliweza kusimama kwa magongo. Nilipewa magongo ya kwapa kusaidia harakati zangu. Hivi sasa ninatumia moja. Afya yangu imeimarika, na nitaendelea kuja hapa kwa tiba ya mwili ili nipate kupona kabisa,” anasimulia Amina.

DSC_0149.JPG

Ali na Noor husaidia watoto na watu wazima ambao wameumia na au wanaisi na ulemavu kupata na kujifunza kutumia viti vya magurudumu, fimbo nyeupe, viti vya choo, vifaa vya kutembea, na magongo.

Zaidi ya utoaji, ukarabati, na utunzaji wa vifaa vya usaidizi na uhamaji, kituo cha ukarabati cha LWF hutoa huduma kama vile:

  • Utoaji wa vifaa vya kuona na kusikia, pamoja na mafuta ya kujikinga na makali ya jua kwa jamii ya albino
  • Kutoa matibabu kupitia shughuli za kila siku (occupational therpahy), tibamaungo, Huduma za Usaidizi wa Kisaikolojia, Tiba za kuweza kuzungumza (speech theraphy) n.k.
  • Utoaji wa vocha mpya za Chakula (FFVs) kwa wanaoishi na ulemavu -watoto na watu wazima - walio katika mazingira magumu ili kuwapa msaada na kukimu mahitaji yao ya lishe bora.
  • Kuwatuma wanaohitaji misaada ya Kimaisha, huduma za Afya, Elimu Jumuishi, Ulinzi, Vitu visivyo vya Chakula, Makao, maji na usafi wa mazingira (WASH), Mkusanyiko Mbadala wa Chakula, nk.
  • Huduma maalum kama vile upasuaji wa kurekebisha na utoaji wa viungo bandia.
  • Msaada wa wanaoishi na ulemavu wwa kupooza mwili wote na vifaa vya utu, magodoro yenye wiani mkubwa kuzuia vidonda ikiwa na mafunzo ya misaada ya jinsi ya kusonga ama kusongeshwa.
  • Huduma za ushauri, tiba ya nyumbani, kuwatembelea wafadhiliwa nyumbani na ufuatiliaji wa kesi zinazohusu ulemavu.

Je! Ungependa kuzungumza na LWF au utafute huduma zao katika Kituo cha Ukarabati cha Jamii huko Dadaab?

Kituo cha ukarabati cha LWF huko Dadaab kiko wazi kwa wateja. Huduma zote zinazotolewa kwa Watu Wenye Ulemavu katika kituo hicho ni BURE. Unaweza kuuliza maswali zaidi juu ya huduma hizi kwa kupiga simu kwa LWF kupitia nambari: 0800721316

Unaweza kutazama hadithi ya Noor na Ali kwenye Ukurasa wetu wa Facebook hapa.

Je, una maswali yoyote? Wasiliana nasi kupitia ukurasa wa Facebook wa Julisha.Info, Jumatatu hadi Ijumaa kutoka saa 2 asubuhi hadi saa 11 jioni.